Wednesday, November 25, 2015

Kama wewe unatafuta ajira, taarifa hii kutoka Secretariate ya Ajira na Utumishi wa Umma Tanzania Inakuhusu

Maelekezo muhimu ya ujazaji wa Taarifa kwenye mfumo wa Recruitment Portal kwa waombaji kazi


 Sekretarieti ya ajira katika utumishi wa Umma imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa utumaji wa maombi ya kazi (Recruitment Portal) ambao humsaidia muombaji kazi kutuma maombi hayo popote alipo ndani na nje ya Nchi kwa njia ya mtandao.
Ni muhimu kuzingatia kuwa kabla ya ujazaji wa taarifa kwenye mfumo wa ajira kila muombaji kazi lazima awe na barua pepe ambayo ni hai(Active email address) ambayo atatakiwa kujisajili katika sehemu iliyoandikwa Register katika ukurasa wa mbele wa mfumo (Home page) kabla ya muombaji kujaza taarifa zake katika vipengele 11 vilivyoelezewa kwenye makala haya. Pia kwa waombaji wote wanatakiwa kuhakikisha taarifa zao zote wanazojaza ni za uhakika na zipo katika ukamilifu.
 
Mfumo huu unapatikana kupitia anuani ya portal.ajira.go.tz ambapo baada ya usajili mwombaji kazi atajaza taarifa zake. Mgawanyo wa taarifa hizo upo katika vipengele vikuu 11 ambavyo ni Taarifa binafsi (Personal Details), Taarifa za Mawasiliano (Contact Details), Sifa za kielimu (Academic Qualifications), Sifa za Kitaaluma (Professional Qualifications), uwezo wa lugha (Language Proficiency), uzoefu wa kazi (Working Experience), Mafunzo, Warsha na Makongamano aliyowahi kuhudhuria (Training & Workshop Attended), ujuzi wa matumizi ya kompyuta (Computer Literacy), wadhamini (Referees), viambatanisho vingine (Other Attachments) na udhibitisho wa taarifa zilizoingizwa (Declaration). Aidha kila kipengele kinapaswa kujazwa kulingana na kinavyojieleza kwa ukamilifu wake.
Kwa kuwa kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya waombaji kazi kutojaza taarifa zao kikamilifu au kujaza baadhi ya taarifa zao kwenye vipengele visivyohusika, makala hii itajikita katika kuelezea kwa kina taarifa gani zinapaswa kujazwa kwa kila kipengele ili kuweka uelewa mpana kwa waombaji kazi kutokana na changamoto ambazo zimekua zikijitokeza kwa baadhi ya waombaji kazi kutozingatia masharti ya ujazaji wa taarifa hizo kikamilifu kwa kila kipengele kabla ya kutuma maombi ya kazi.  
Wapo baadhi ya waombaji kazi ambao wamekuwa wakijaza taarifa ambazo hazihusiani na kipengele husika hali inayoleta changamoto katika uchambuzi wa taarifa zao kwenye mfumo. Kwa kuzingatia changamoto hiyo na ili kukuza uelewa zaidi kwa waombaji kazi kupitia mfumo huo, yafuatayo ni maelezo muhimu yanayotakiwa kujazwa kwa kila kipengele kilichopo kwenye mfumo.
Personal Details (Taarifa binafsi)
Kipengele hiki kinatakiwa kujazwa taarifa za binafsi ambazo ni majina matatu, jinsia, uwepo/kutokuwepo kwa hali ya ulemavu, Uraia, tarehe na mahali pa kuzaliwa, hali ya ndoa, rekodi ya makosa ya jinai (kama mhusika anayo) na miaka ya uzoefu wa kazi (years of working experience).
Contact Details (Taarifa za Mawasiliano) 
Katika Kipengele hiki, muombaji anatakiwa kujaza anuani ya posta kwa wakati huo, Nchi anayoishi, Mkoa, Wilaya, anuani ya kudumu ya posta, namba za simu za mwombaji pamoja na barua pepe ya ziada ambayo mwombaji kazi anaitumia. 
Academic Qualifications (Sifa za kielimu)
Hiki ni kipengele muhimu ambacho mwombaji kazi anapaswa kujaza taarifa zake zote za kitaaluma ambazo ni pamoja na cheti cha kidato cha nne, kidato cha sita, Astashahada (Certificate), Stashahada (Diploma), stashahada ya juu (advanced diploma), shahada (Degree), Shahada ya uzamili (Master’s Degree), Shahada ya Uzamivu (Phd) na kuendelea kulingana na kiwango cha elimu ya juu mhusika aliyofikia. 
Aidha kitika kipengele hiki cheti halisi cha taaluma iliyojazwa ni lazima kiambatishwe katika sehemu iliyoandikwa Attach to update your certificate. Mjazajia au muombaji kazi anapaswa kuhakikisha kwamba vyeti vya elimu vyote vimekuwa ‘scanned’ vikiwa nakala moja moja (yani visiwekwe vikawa ‘document’ moja) na kuvihifadhi katika mfumo wa pdf. Pia ni muhimu kuzingatia kuwa leaving certificate, Results Slip au Partial transcript haziruhusiwi kuwekwa katika kipengele hiki isipokua vyeti halisi pekee.
Professional Qualifications (Sifa za Kitaaluma)
Kipengele hiki ni tofauti kabisa na kipengele kinachohusu academic Qualification (Sifa za kielimu). Professional Qualification inahusu vyeti vya kitaaluma ambavyo vinatolewa na bodi mbalimbali. Kwa mfano taaluma kama za uhasibu au Ukaguzi wana vyeti vya kitaaluma vinavyotolewa na Bodi ya Taifa ya wahasibu na wakaguzi (NBAA), Taaluma za Uhandisi (engineering) wana vyeti vya Kitaaluma kutoka katika Bodi ya usajili wa makandarasi na uhandishi (ERB) pamoja na taaluma nyingine zenye utaratibu kama huo. Kwa maana hiyo katika kipengele hiki viambatishwe vyeti vinavyotolewa na bodi za kitaaluma na sio vinginevyo. 
Kwa kuwa si kila kada/Taaluma ina vyeti vinavyotolewa na bodi maalum, si waombaji kazi wote watakaoweza kujaza kipengele hiki. Hivyo basi ujazaji wa kipengele hiki hakiwahusu waombaji kazi wa kada zote. Pia vyeti vya shahada na stashahada ya juu havitakiwi kuwekwa hapa bali katika Academic qualifications.
Language Proficiency (Uwezo wa lugha)
Kipengele hiki kinamtaka mwombaji kazi aainishe uwezo wake wa lugha mbalimbali katika kuongea, kuandika na kusoma. Lugha hizi ni kama vile Kiswahili, kiingereza na kadhalika. 
Working Experience (uzoefu wa kazi)
Katika kipengele hiki muombaji kazi anapaswa kuweka taarifa za uzoefu wa kazi alionao. Kwa waombaji waliotoka vyuoni na hawajawahi kupata kazi waweke taarifa za mafunzo kwa vitendo (Field practical training) ambayo wamefanikiwa kufanya wakiwa chuoni au baada ya kuhitimu. 
Training & Workshop Attended (Mafunzo, Warsha na Makongamano aliyohudhuriwa)
Sehemu hii mhusika anapaswa kujaza sehemu au taasisi aliyopata mafunzo husika, kuambatanisha vyeti vya mafunzo na warsha husika alizowahi kuhudhuria (kama zipo). Mfano mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), mafunzo au semina ya uongozi, ujasiriamali, biashara, masoko. Kama muombaji kazi hajapata mafunzo au warsha yoyote si lazima kujaza kipengele hicho.
Computer Literacy (ujuzi wa matumizi ya kompyuta)
Katika eneo hili muombaji anapaswa kujaza ujuzi wake wa kutumia Kompyuta (kama ujuzi huo anao) pamoja na kujaza aina ya ujuzi alionao (Mfano MS Word, MS Excel, MS Power point) pamoja na kuambatisha vyeti vya mafunzo hayo kama mhusika anavyo.
Referees (wadhamini)
Kila muombaji fursa za ajira anatakiwa kuweka wadhamini watatu ambao wanaweza kudhibitisha taarifa zilizowekwa. Wadhamini hawa wawe watu wanaowajua waombaji hawa na kuweza kupatikana kwa ajili ya kutoa maelezo kuhusiana na elimu, tabia, uzoefu wa kazi, n.k. Taarifa za kuweka ni majina, namba ya simu, anuani ya barua pepe na mahala wanapofanya kazi.
Other Attachment (viambatanisho vingine)
Katika kipengele hiki muombaji kazi anapaswa kuambatanisha cheti cha kuzaliwa, maelezo binafsi (CV) na vyeti vya uhakiki kwa waombaji waliosoma nje ya Tanzania kutoka mamlaka husika (TCU na NECTA).
Declaration (udhibitisho wa taarifa zilizoingizwa)
Hiki ndicho kipengele cha mwisho katika ujazaji wa taarifa ambapo mwombaji kazi anapaswa kutoa uthibitisho wa taarifa alizojaza kuwa ni sahihi kwa uelewa wake kwa kutambua kuwa kama atatoa au kujaza taarifa za uongo maombi yake ya kazi hayatafanyikiwa katika mchakato wa uchambuzi wa waombaji kazi. 
Ili kuhakikisha mchakato wa kuomba kazi kwa mfumo huu unafanyika kwa urahisi na uharaka zaidi, ni vyema kwa muombaji kuhakikisha vyeti vyake vyote vinavyohitajika viwe ‘scanned’ na kuhifadhiwa katika mfumo wa pdf. Picha za passport size pia zinaweza kuwekwa katika mfumo wa gif au jpg lakini ziwe na kb ndogo (yani ‘size’ ndogo).
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
Kwa maelezo zaidi wasiliana nasi kwa namba 0784 398259 au 0687 624975.
SOURCE: UTUMISHI

0 comments:

Post a Comment