Watu 1,000 nchini
Sierra Leone wamewekwa kwenye karantini baada ya kugunduliwa kuwa
mwanamke wa umri wa miaka 67 alifariki kutokana na Ebola.
Hilo limejiri siku tano tu baada ya kuanza kwa hesabu ya wiki sita iliyolenga kutangaza taifa hilo kuwa bila Ebola.
Karantini hiyo itadumu wiki tatu, mradi tu kusiwe na visa vipya vitakavyoripotiwa.
Watu Zaidi ya 11,000 wamefariki tangu kuanza kwa mkurupuko wa Ebola nchini Sierra Leone, Guinea na Liberia.Maafisa wa
serikali nchini humo walikuwa na matumaini baada ya kupita kwa kipindi
kirefu bila kisa kipya cha Ebola na kwamba kisa cha sasa kimewashangaza.
Mwandishi
wetu anasema karantini ya sasa ina masharti makali zaidi kuliko za
awali. Ni pamoja na amri ya kuzuia watu kutembea kutoka nyumba moja hadi
nyingine.
Wanajeshi na maafisa wa polisi wametumwa kudumisha
karantini hiyo katika kijiji cha Sellakaffta, kilichoko Kambia kwenye
mpaka wa kaskazini wa taifa hilo na Guinea.
Maafisa wa Shirika la
Afya Duniani na wizara ya afya Sierra Leone wanapanga kutoa chanjo kwa
wale ambao huenda walikutana na mwanamke huyo.
Guinea inajaribu
kudhibiti mkurupuko wa ugonjwa huo nchini humo. Liberia, WHO ilitangaza
kuwa virusi vya Ebola vimeacha kusambaa kwa mara ya pili Alhamisi.
Taifa hilo lilitangazwa kutokuwa na Ebola mwezi Mei lakini visa zaidi vikaripotiwa mwezi uliofuata.
SOURCE:BBC SWAHILI.
0 comments:
Post a Comment