Wednesday, January 28, 2015

Kisa Cha Marafiki Watatu: Julius, Oscar Na Rashid..


 Ndugu zangu,

Nimeandika huko nyuma, kuwa watatu hawa, Julius Nyerere, Oscar Kambona na Rashid Kawawa, kuwa ndio walikuwa Watanganyika wenye nguvu na ushawishi mkubwa kwenye Tanganyika Huru.
Nchi ilikuwa changa, na viongozi nao walikuwa wachanga sana. Nyerere alikuwa mbele yake na dhamana kubwa aliyoibeba.
 

Nchi ilihitaji kujitambua, kisha kusonga mbele. Nyerere, mwalimu wa kawaida, ambaye hakupata hata kuwa Headmaster pale Pugu Sekondari, anaambiwa, kuwa sasa wewe ni Head Of State - Mkuu Wa Nchi.

Na wakati huo Dunia ilikuwa kwenye Vita Baridi. Iligawinyika kati ya Ubepari na Ukomunisti. Nyerere haliona, kuwa hatuwezi kuwa nchi ya kibepari, lakini, hatuwezi pia kuwa nchi ya Kikomunisti. Nyerere alialikwa Marekani, akafika China pia. Kuna mazuri aliyaona Marekani, na mazuri aliyaona China.


Nyerere aliamini katika Ujamaa wa Kiafrika- African socialism. Katika hilo, Rashid alimwelewa, lakini, Oscar alichagua kuwa Tomaso. Ishara za Oscar na Julius kutofuata njia moja zilianza kuonekana. Na safari yao ya Uchina ilionyesha, ni jinsi gani, wawili hao waliangalia China kwa miwani tofauti.(P.T)

Julius aliona nini China?
Julius alivyutiwa sana Kiongozi Mkuu Mao. Aliona kuna mengi yanayofanana kati ya China na Tanzania.

Vile Mao alivyowakusanya Wachina kwenye vijiji ilirahisisha kuwafikishia ujumbe kwenye mapambano dhidi ya njaa, umasikini na maradhi. Kwamba ndio njia nzuri ya kuifanya nchi kujitegemea kwa watu wake kushiriki kazi za uzalishaji kijamaa. Lakini pia, kuondokana na sauti zenye kupinga; hivyo kuondokana na upinzani.

 Na Julius akikumbuka mkutano ule mgumu na Balozi wa Marekani pale Dar, Julius alianza kuiona njia ya kuachana kabisa na Wamarekani. Pamoja na kumwagiwa sifa na John Kennedy alipotembelea White House kwa mara ya kwanza. Julius aliuona ugumu wa kufanya kazi na Wamarekani.
Oscar aliona nini China?

Oscar hakuvutiwa kabisa na Mao. Hakuamini kuwa njia ya Mao ni sahihi pia kufuatwa na Tanzania. Kwenye moja ya kumbukumbu ya ziara yao ya China, kumbukumbu ambazo Oscar hakupata kuzichapisha, anasema; " Mao anafanywa kama Mungu. Kutukuzwa kwa Mao hakukumshtua Nyerere, hakuna alichohoji. Mao anakuwa mfano wa kuigwa kwa Nyerere. Na Nyerere anabadili hata staili ya mavazi yake." ( Oscar Kambona, Pa vag till presidenten, ukurasa wa 200)

Oscar alikubaliana na Julius kuwa Chama kimoja kinaweza kuwa mkakati mzuri kuzuia mgawanyiko wa kikabila na kimaslahi kama inavyotokea mara nyingi katika nchi za Afrika, na hilo la mwisho walikubaliana lisitokee. Mara baada ya kurudi kutoka China, haikupita muda, Tanzania ikafanywa kuwa nchi ya Chama kimoja.

Tangu hapo, dalili za marafiki wawili kuanza kufarakana zikaanza kudhihiri. Na hiki hasa kikawa ni kisa cha marafiki watatu waliogundua kuwa mmoja wao ana mtazamo tofauti. Na hakika, mtazamo wa sera za Kibepari aliokuwa nao Kambona kwa wakati ule, kama ungetekelezwa kwenye Tanganyika mpya, basi, mwelekeo wa nchi ungebadilika sana. Wanyonge wengi wangeachwa nje ya mfumo ule. Maana, Watanganyika walikuwa hawajaandaliwa kupambana katika mazingira ya kibepari.

Kuondoka kwa Oscar kulitoa nafuu ya Julius na Rashid, kuifanya kazi ya Ujenzi wa Umoja wa Kitaifa, wakiamini pia, kuwa ndio nguzo ya maendeleo.
Simulizi ya kisa cha marafiki watatu hawa yaweza kuwa ndefu. Na ajabu ya marafiki watatu hawa; Kambarage ( Julius) Kawawa( Rashid) na Kambona ( Oscar), wote watatu wana majina ya pili yenye kuanzia na herufi ' K'.

Na ili tufahamu zaidi urafiki wa watatu hawa ni vema tufahamu jinsi walivyokutana;
Nyerere alikutana na Oscar Kambona wakati Kambona alipokuwa shuleni Tabora mwishoni mwa miaka ya 40. Inasemwa, kuwa Nyerere alimtangulia kiumri Oscar kwa kupishana miaka mitatu tu. Kule Tabora Nyerere alikutana pia na Rashid Kawawa, naye alimzidi kiumri kwa miaka mitatu hivi.
Hivyo basi, twaweza kusema, kuwa urafiki wa Julius, Oscar na Rashid ulianzia Tabora, na harakati zao za pamoja za mapambano ya kisiasa zilianzia huko huko Tabora.
Ni nini basi kilifuatia kwenye urafiki wao ? Nitasimulia zaidi nikipata wasaa...
Maggid Mjengwa 
kutoka
Mjengwa blog

0 comments:

Post a Comment