Rais Vladmir Putin wa Russia amesema leo kuwa, mgogoro wa
wahajiri unaolikabili bara Ulaya kwa sasa umetokana na sera mbovu za
kigeni za nchi za bara hilo hususan zile ambazo ni wanachama wa Umoja wa
Ulaya (EU). Kiongozi huyo amesisitiza kuwa, uingiliaji wa Wamagharibi
katika mambo ya ndani nchi za Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika
ni moja ya sababu za kuibuka mgogoro wa wahajiri katika nchi za EU.
Rais Putin amesema viongozi wa Ulaya wameingia kwenye mtego wa
Marekani kwa kukubali kufuata kibubusa sera zake hususan katika
ulimwengu wa Kiislamu na kwa mantiki hiyo migogoro ya kisiasa katika
nchi za Syria, Libya, Somalia, Yemen na kwingineko imewafanya raia wa
nchi hizo kukimbilia usalama wao barani Ulaya. "Wanawatwisha watu sera
zao kwa lazima bila ya kujali itikadi zao za kidini, utamaduni wao na
muundo wa jamii. Hilo lazima litaleta matatizo makubwa", amesema
kiongozi huyo. Rais wa Russia ametahadharisha kuwa, EU na Marekani
zisipobadili sera zao za kigeni mgogoro huo utakuwa mpana zaidi katika
siku za usoni.
SOURCE: TEHRAN
0 comments:
Post a Comment