Miroslav Klose amevunja rekodi ya Ronaldo na kuwa mfungaji mwenye mabao mengi zaidi katika historia ya fainali za kombe la dunia.
Mshambuliaji huyo wa Ujerumani alifunga bao la pili katika ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Brazil kwenye mchezo wa nusu fainali wa kombe la dunia na kufikisha mabao 16.
Lilikuwa bao lake la pili katika mashindano baada ya kufunga bao akitokea benchi katika mchezo dhidi ya Ghana, hatua ya makundi na kumfanya alingane mabao na gwiji wa Brazil. Wafungaji waliofunga magoli mengi zaidi katika mashindano ya kombe la dunia muda wote ni pamoja na Miroslav Klose 16, Ronaldo De Lima 15 , Gerd Muller 14, Just Fontaine 13, Pele 12, Jurgen Klinsmann 11, Gary Lineker 10.
Klose alicheza kwa mara ya kwanza fainali za kombe la dunia mwaka 2002 na kufunga mabao matatu `hat-trick` katika ushindi wa mabao 8-0 dhidi ya Saudi Arabia.
Alifunga tena bao katika mechi iliyofuata ya makundi ambayo Ujerumani ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Ireland, kabla ya kufunga bao la pili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Cameroon.
Licha ya Ujerumani kufika fainali mwaka ule, Klose alishindwa kufunga tena katika mashindano, akimaliza michuano kwa idadi sawa ya mabao na Rivaldo, nyuma ya mfungaji bora, Ronaldo aliyefunga mabao 8.


