Monday, June 22, 2015

Jaji Warioba asema kitu juu ya wagombea urais CCM


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amewashangaa makada wanaojinadi kuwa ni wasafi na waadilifu, akisema sifa hizo zinatakiwa zitolewe na jamii.
Jaji Warioba, mmoja wa watu ambao wamekuwa wakikemea masuala ya ukiukwaji wa maadili, pia amesema hatamuunga mkono mgombea ambaye anakiuka maadili ya uongozi.
Tayari makada 37 wamejitokeza kuomba ridhaa ya wana-CCM kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wengi wao wamekuwa wakijinadi kuwa ni wasafi na waadilifu na kuwataka wanachama kutowapitisha watu wenye harufu ya ufisadi na wasio waadilifu.
Lakini Jaji Warioba alisema anaona wanakwenda kinyume na inavyotakiwa kufanyika.
“Viongozi wa sasa wanaonekana hawajali misingi ya maadili kwa sababu jamii yetu yenyewe imeonyesha kutochukizwa na suala hili la mmomonyoko wa maadili na wala jamii haijalipa uzito unaostahili,” alisema Jaji Warioba wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Vuguvugu la uhuishaji wa Maadili kwa Jamii (Moral Rivival Movement).

“Viongozi wengi waliochukua fomu za kugombea urais wanaonekana kujitangaza kuwa wao ni waadilifu. Jamii ndiyo ilipaswa kusema kuwa viongozi hao ni waadilifu au sio waadilifu na sio wao kujinadi,” alisema Warioba ambaye pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu.
Mkutano huo ulioandaliwa na viongozi wa dini kwa kushirikiana na Chama cha Wataalamu wa Wakikristo (CPT) ulijadili ujenzi mpya wa maadili katika jamii utasadia kupata kiongozi mwenye misingi ya maadili ili kuepuka mitafaruku baina ya siasa za madaraka na siasa za maslahi.
“Nimekuja hapa leo (jana) kuwaunga mkono katika uzinduzi wa Vuguvugu la Uhaishaji Maadili kwa Jamii kwa sababu na mimi ni sehemu ya mapambano hayo. Sitaunga mkono ng’o kiongozi yeyote ambaye ataonekana kutokuwa na misingi ya maadili ya uongozi katika kipindi hiki cha uchaguzi,” alisema Jaji Warioba.
Warioba, ambaye alieleza kuwa ameamua kukaa kimya kuhofia kila anachosema kuhusishwa na masuala ya uchaguzi, alisema viongozi ambao hawana maadili wamechangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa mianya ya rushwa.
“Lakini kama tunataka kuwa na viongozi wenye misingi ya maadili, ni lazima tujenge upya maadili kwa sababu tusipofanya hivyo yatazidi kuporomoka,” alisema waziri mkuu huyo wa zamani.
Azungumzia suala la ubaguzi:
“Tumeona sasa ukabili umeanza kurudi, ubaguzi wa kidini umeanza kurudi, ubaguzi wa kikanda umeanza kurudi, ubaguzi wa namna hii umeanza kurudi kutokana na kukosekana kwa maadili,” alisema Jaji Warioba ambaye alitumia muda mwingi kuishauri jamii kufuata misingi ya maadili iliyoachwa na waasisi.Profesa Beda Mutagahywa anena:
Akizungumzia maana ya Uhuishaji maadili( MRM), Profesa Beda Mutagahywa alisema ni hamasa ya umma kwenda mbele kufikia malengo fulani ya kijamii na malengo hayo yapo, yalikuwepo lakini hamasa ya kuyafikia ilififia na hatimaye malengo yakasahaulika.
“Hii itasadia kama tutafanikiwa kuufanya uwe ajenda na sehemu ya ilani ya vyama mbalimbali vya siasa katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema.
Source: Mjengwa blog via Mwananchi

0 comments:

Post a Comment