Tuesday, September 8, 2015

Kenya yaanzisha operesheni kuzima Alshabab

Rais Kenyatta amemuagiza inspekta mkuu wa polisi kuendesha operesheni dhidi ya ugaidi.


Operesheni hiyo inayoendeshwa na vikosi maalum vya kupambana na ugaidi kwa ushirikiano na jeshi la taifa linalenga wapiganaji takriban mia tatu wa Jeysh al Ayman wanaosadikika kujificha katika msitu huo. Kundi hilo la Jeysh al Ayman linasadikiwa kuwa na uhusiano na wapiganaji wa Al Shabaab
Msemaji wa shirika la msalaba mwekundu katika eneo la Lamu na Kilifi Bwana Musa Hassan, ameliambia gazeti la The Standard kuwa asilimia kubwa ya watu wanaotoroka ni wakaazi wa eneo la Basuba na wengine walioko Kusini mwa Garissa wanaohofia kupatikana katikati ya makabiliano yanayotarajiwa kati ya wanamgambo hao na vikosi vya usalama vya Kenya.
Wizara ya usalama ilitoa ilani mwishoni mwa juma ikiwataka wakaazi wa maeneo yanayopakana na msitu huo ikiwataka watu wote wanaomiliki bunduki katika eneo hilo kuzisalimisha kabla ya kuanza kwa operesheni hiyo inayohusisha vikosi vya wanahewa na wale wa nchi Kavu.



 
Manuari za kijeshi zilionekana zikiingia Boni
Tayari idadi kubwa ya vikosi vya jeshi vimeripotiwa kuonekana katika maeneo ya Mangai, Baure,Kaskazini mwa Lamu, Bodhai na Hulugho.
Mkuu wa polisi katika eneo la Ijara Christopher Rotich amenukuliwa akithibitisha kuwepo kwa mipango hiyo ya kudhibiti utovu wa usalama unaotokana na mashambulio ya mara kwa mara yanayodaiwa kutekelezwa na kundi hilo la wanamgambo la wa Jeysh al Ayman.
Kundi hilo lanalosemekana kujumuisha wenyeji linalaumiwa kwa jaribio la kuvamia kambi ya kijeshi iliyoko Baure mwezi juni.
Aidha kundi hilo ndilo linalodaiwa kutekeleza shambulizi la bomu la kutegwa ardhini mapema mwaka huu.


 
Majuzi tu kundi hilo linadaiwa kuvamia wanakijiji wa Basuba na kutoa hutuba kwa muda mrefu mbali na kuwaonya wenyeji dhidi ya kutoa habari na kushirikiana na polisi.
Inspekta mkuu wa polisi wa Kenya, Joseph Boinnet, alitangaza hali ya tahadhari katika maeneo ya msitu wa Boni huku akitoa amri ya kuitangaza Boni kuwa eneo la Operesheni.
Msitu huo mkubwa wa Boni upo katika majimbo tatu nchini Kenya ya Lamu, Garissa na Tana River.
Aidha unapakana na bahari Hindi kuanzia Lamu hadi mpaka wa Kenya na Somalia.
SOURCE: BBC SWAHILI

0 comments:

Post a Comment