Wednesday, December 17, 2014

NAPE APONGEZA WAPINZANI

NapeNnauye_480_280_2238a.jpg

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimevipongeza vyama vingine vya siasa nchini kwa ushiriki wao kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwataka waongeze kasi kwani ushindi wao wa asilimia 14 hadi sasa ni mdogo, ukilinganisha na umri wa mfumo wa vyama vingi nchini ambao ni miaka 20.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Nape Nnauye alisema vyama vya upinzani vinapaswa kupongezwa kwa kushiriki kwenye uchaguzi huo na kwamba kwa maeneo waliyoshinda wanapaswa kuwaletea maendeleo wananchi, ili wasipoteze imani kwao.

Alisema pamoja na ushindi huo, vyama hivyo visitarajie mabadiliko makubwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwakani wa madiwani, wabunge na Rais, kwani pamoja na kupata asilimia hizo 14, hali haitabadilika ukilinganisha na ushindi wa CCM.

“Ni kweli pamoja na kwamba uchaguzi kama huu uliopita CCM ilishinda kwa asilimia 96 na mwaka huu kwa asilimia 84, bado sio kigezo cha vyama vya upinzani kufanya vizuri zaidi ya asilimia hizo 14 walizoambulia hadi sasa kwa maeneo ambayo matokeo yametoka”, alisema Nape.

Alisema hata maeneo ambayo uchaguzi utarudiwa, sio rahisi vyama hivyo kupata ushindi wa kishindo, kwani hadi sasa wameshaona mwelekeo wa kukubalika kwao kwa wananchi.
Alisema kwa matokeo hayo, vyama vya upinzani zinapaswa kuongeza kasi kwani tangu mfumo wa vyama vingi uanze kutumika nchini ni miaka 20 sasa na bado vyama hivyo havijakua ipasavyo. 
Source: Mjengwa blog

0 comments:

Post a Comment