Transparency International yasema rushwa ni tatizo kwa wote
Riport na DW
Katika ripoti yake ya leo (03.12.2014) shirika hilo lilisema rushwa
inaonekana kukithiri Uturuki na China na limetaka kuwepo ushirikiano wa
karibu wa kimataifa kuangamiza kabisa rushwa na matumizi mabaya ya
madaraka.
Katika ripoti yake shirika la Transparency International hilo lenye
makao yake Berlin Ujerumani lilisema rushwa ni tatizo kwa uchumi na kuna
umuhimu wa taasisi kubwa za fedha katika Umoja wa Ulaya na Marekani
kufanya kazi pamoja na nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi kuwakomesha
mafisadi wasikwepe mkono wa sheria.
Katika faharasa ya 20 inayoonyesha viwango vya rushwa katika mataifa
175, China imepata alama 36 kati ya 100, Uturuki imepata 45 na Angola
19, zikiwa nchi ambazo zimeanguka kwa alama kati ya 4 na 5, licha ya
uchumi wao kukua kwa wastani wa asilimia 4 katika kipindi cha miaka
minne iliyopita. Transparency International hutoa alama 100 kwa nchi
ambayo haina visa vya rushwa na sufuri kwa nchi ambayo rushwa
imeshamiri.
Kwa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki, Rwanda imefanya vyema katika
kupambana na rushwa ikishikilia nafasi ya 55, ikifuatiwa na Tanzania
katika nafasi ya 119, na Uganda ni ya tatu katika nafasi ya 142. Kenya
ni ya nne katika nafasi ya 145 na Burundi inashika mkia katika jumuiya
ya Afrika Mashariki ikiwa katika nafasi ya 159.
Zaidi ya theluthi mbili kati ya nchi 175 katika faharasa hiyo
zimepata pointi chini ya 50 huku Somalia, Korea Kaskazini, Sudan,
Afghansitan na Sudan Kusini kwa mara nyingine tena zikishika nafasi za
chini.
Mkurugenzi wa Transparency International katika mataifa yaliyo kusini
mwa jangwa la Sahara, Chantal Uwimana, alisema, "Vipindi vya mizozo
huchochea rushwa, kuyumba kwa hali ya kisiasa na kukosekana uthabiti kwa
sababu mifumo hudhoofika au wale wanaotakiwa kuisimamia mifumo hii
wanapoteza muelekeo.Si jambo la kushangaza kwamba Sudan Kusini na
Somalia ambazo zimekabiliwa na vita kwa muda mrefu zinaonekana kuwa na
vitendo vya rushwa iliyokithiri."
Denmark ni mfano wa kuigwa
Nchi iliyofanya vizuri kabisa na kushika nafasfi ya kwanza ni Denmark
ikijipatia pointi 92, ikifuatiwa na New Zealand, Finland, Sweden na
Norway, zote kwa mara nyingine tena zikiwa katika tabaka la nchi tano za
kwanza aktika faharasa ya rushwa.
Ukraine ilipata pointi 26 na kubakia kuwa nchi inayoongoza kwa
kiwango kikubwa cha rushwa barani Ulaya. Italia,Ugiriki na Romania kwa
pamoja zimafanya vibaya miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya
zikiwa na pointi 43.
Mwenyekiti wa Transparency International, José Ugaz alisema maafisa
mafisadi huficha mali walizozipata kwa njia isiyo halali na kuzificha
katika maeneo salama kupitia kampuni. Ugaz aidha amesema ufisadi mkubwa
katika nchi zenye uchumi mkubwa haukandamizi tu haki za binadamu kwa
watu masikini, bali pia husababisha matatizo ya utawala na uthabiti.
Ripoti hiyo ilizitaka nchi zinazoshika mkia katika orodha
iliyochapishwa zichukue hatua madhubuti za makusudi kupambana na rushwa
kwa masilahi ya umma. Ugaz aliyataka mataifa yanayoshika nafasi za juu
katika faharasa hiyo yasieneze vitendo vya ufisadi katika nchi ambazo
hazijaendelea.
Shirika la Transparency International liliuhimiza Umoja wa Ulaya,
Marekani na kundi la G20 la mataifa yaliyostawi na yanayoinukia
kiuchumi, kuiga mfano wa Denmark na kuanzisha daftari la umma
linalojumuisha tarifa muhimu za wamiliki kwa kampuni zote
zilizoshirikishwa.
0 comments:
Post a Comment