Friday, December 19, 2014

Jumuiya ya Ulaya yaungana dhidi ya Russia



Viongozi wa Ulaya wamemaliza kikao chao mjini Brussels Ubelgiji, wakisema kwa sasa wameungana zaidi kuliko ilivyokuwa awali katika kuikabili Urusi. Viongozi hao wameonesha kuwa vikwazo vya kiuchumi havitadhoofishwa licha ya matatizo ya kifedha yanayoikabili Urusi.

Badala yake hatua mpya za Umoja wa Ulaya zilizokuwa zimewekwa kufuatia Urusi kulitwaa kimabavu jimbo la Crimea zimepitishwa na zitaanza kutumika mwishoni mwa wiki hii.

Rais mpya wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk akifunga kikao cha viongozi wa EU amesema Urusi na vitendo vyake ni tatizo kubwa la kimkakati linaloikabili Ulaya.

Akiongoza kikao cha wakuu wa nch ishirini na nane za Umoja wa Ulaya. Bw. Tusk amesema kuwa vitendo vya Urusi ndani ya Ukraine na katika Ulaya ni changamoto na alibaini kwamba mataifa ya Umoja wa Ulaya yameungana zaidi kuliko ilivyowahi kuwa huko nyuma katika kukabiliana na Urusi.

Aidha, ameonya kuwa Ulaya inahitaji mkakati wa muda mrefu wa aina yake,ambao si tu utakaoshughulikia matatizo katika wiki zijazo na miezi, bali miaka. Wakati huo huo viongozi wamekubaliana vikwazo vipya vinavyopiga marufuku uwekezaji katika jimbo la Crimea, ishara kwamba vikwazo hivyo havitalegezwa hadi Urusi itakapobadili msimamo wake kuhusu jimbo hilo.
Source: BBC

0 comments:

Post a Comment